UJENZI RASMI BOMBA LA MAFUTA KUANZA MEI

Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Nishati na Kampuni ya Total wamekubaliana kuharakisha hatua zote za awali katika Mradi wa Bomba la Mafuta kutoka Uganda hadi Hoima-Tanga ili shughuli za ujenzi rasmi zianze mwezi Mei mwaka huu.

Makubaliano hayo yalifikiwa jana, wakati Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani alipokutana na uongozi wa juu wa kampuni hiyo wizarani mjini Dodoma.

Aidha, makubaliano mengine yaliyofikiwa katika kikao hicho ni kuwa, kazi za awali za maandalizi ya ujenzi ziwe zimekamilika ifikapo mwezi Machi mwaka huu.

"Ni lazima tuharakishe mchakato huu kama Mheshimiwa Rais Magufuli alivyoagiza. Hivyo, tumekubaliana kwamba shughuli zote za maandalizi ziwe zimekamilika ifikapo Machi mwaka huu ili kuwezesha shughuli rasmi za ujenzi wa Bomba kuanza mwezi Mei," alifafanua Waziri Kalemani.

Vilevile, katika kikao hicho, Rais wa Kampuni ya Total, Sehemu ya Afrika, Guy Maurice ambaye alikuwa kiongozi wa Ujumbe huo, alibainisha nia ya kampuni yake kuwekeza katika shughuli nyingine mbalimbali zinazohusiana na Mradi wa Bomba, jambo ambalo alisema litainufaisha zaidi Tanzania.

Mbali na makubaliano yote yaliyofikiwa, Waziri Kalemani pia alisisitiza kuwa ni muhimu kampuni ya Total iwasilishe Mpango-Kazi wake wizarani mapema iwezekanavyo ili utumike kama mwongozo-rejea katika kutathmini utekelezaji wa Mradi huo mkubwa.

Kampuni ya Total ndiyo mwekezaji katika utekelezaji wa Mradi wa ujenzi wa Bomba la Mafuta kutoka Uganda hadi Hoima-Tanga.

Kikao hicho pia kilihudhuriwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt. Hamisi Mwinyimvua, Kamishna wa Nishati na Masuala ya Petroli Mhandisi Innocent Luoga, Mkurugenzi wa Utawala na Utumishi Lusius Mwenda, Mkurugenzi wa Sera na Mipango Haji Janabi na maafisa wengine waandamizi kutoka wizarani.

Maoni