UVCCM CHAMAZI  YAVUNA WANACHAMA WAPYA 1000 KWA KIPINDI CHA MIEZI SITA. 

Umoja wa Vijana wa Chama Cha  Mapinduzi Kata ya Chamazi jana Jumatano ulifanya sherehe ya kumbukizi ya siku ya wapendanao (valentine day) kwa kujumuika na wanachama wa Umoja huo sambamba na kupokea wanachama wapya 1000.

Sherehe hizo zilizokuwa na lengo la kudumisha mahusiano bora kati ya wanachama wa Umoja huo na viongozi wa UVCCM ngazi ya Kata sambamba na kutoa kadi kwa wanachama wapya zilifanyika katika Tawi la Kisewe.

Sherehe hizo zilianza kwa mchezo wa mpira wa miguu uliokutanisha viongozi na wanachama wa UVCCM mashabiki wa timu za Yanga na Simba, ambapo YANGA WALISHINDA KWA PENATI 4 - 2 na baadaye saa moja jioni kufuatiwa na tafrija fupi.
.


Akizungumza wakati wa sherehe hiyo Mstahiki Meya wa Manispaa ya Temeke Ndg. Abdallah Chaurembo alisema anatambua na kuthamini juhudi za kutafuta wanachama wapya kila kukicha zinazofanywa na Jumuiya ya Vijana ya Chama Cha Mapinduzi Kata ya Chamazi na kuwataka waendelee na moyo huo huo.

"Kwa kweli juhudi zenu naziona, mnafanya kazi kubwa sana ya kuhakikisha Jumuiya inakuwa imara, nimefurahi kuona Vijana wengi katika sherehe hii" alisema Chaurembo.

"Tangu muingie madarakani mmekuwa mkijitahidi kutafuta wanachama wapya kwa njia mbalimbali kutoka kwa wasio na chama na waliokuwa vyama vya upinzani, hongereni sana" alisema Chaurembo.

"Nimefarijika sana kusikia kwa kipindi cha miezi sita (tangu Mwezi wa nane 2017 mpaka sasa mwezi wa pili 2018) mmefanikiwa kupata wanachama wapya elfu moja (1000) hiki ni kitu cha kupongezwa sana kwani msingi wa Chama chochote  Cha siasa ni watu, nanyinyi mmeweza kuwashawishi vijana zaidi ya 1000 kujiunga na  Chama chetu tena kwa muda mfupi, mnastahili pongezi sana" alisema Chaurembo. 

Sambamba na hilo Mheshimiwa Chaurembo aliwataka wanachama wa Umoja huo kukipenda, kukipigania na kukitetea Chama Cha Mapinduzi na kuwahakikishia kuwa Chama hicho kinawapenda na kuwakumbuka Vijana.

Pia sherehe hizo zilihudhuliwa na Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Mkuranga Ndg. Ally Mohammed maarufu Dogo Mambo, Katibu wa UVCCM Wilaya ya Mkuranga  Ndg. Hanzurun Mtebwa sambamba na Mjumbe wa Halmashauri kuu wa UVCCM Wilaya hiyo Ndg. Miraji Punje

Akizungumza baada ya sherehe hiyo mmoja wa wanachama wapya wa umoja huo Ndg. Ally Nassoro alisema amefurahi sana kuona uongozi wa UVCCM wa Kata hiyo ukiwajali wanachama wake katika kipindi hiki ambacho sio cha uchaguzi kwani imekuwa kasumba kwa viongozi wa vyama kuwathamini wapiga kura kwa kuwapa pesa na kofia kipindi cha uchaguzi pekee. 

Pia Ndg. Nassoro ameahidi kuwa balozi mzuri wa Chama Cha Mapinduzi kwa kuwahamasisha Vijana wengine kujiunga na Chama Cha Mapinduzi.


Mstahiki Meya Manispaa ya Temeke Ndg Abdallah Chaurembo akicheza mziki na Mwenyekiti wa Uvccm kata ya chamazi Ndg Nasri Mkalipa. 
Baadhi ya vijana wa Uvccm  kata ya chamazi. 
Vijana wa Uvccm kata ya chamazi wakiwa wanawatazama viongozi Meza Kuu. 

Maoni