WAKULIMA WA VIAZI IPELELE "WAMWAGA MACHOZI"

Wakulima wa viazi katika kata ya Ipelele tarafa ya Magoma wilayani Makete mkoani Njombe wamesema kuwa wamekuwa wakikabiliwa na changamoto kubwa ya soko la uhakika, viazi vinapokuwa vimefikia hatua ya kuuzwa kwani mara nyingi huwatumia madalali ambao hupanga bei wanazozitaka wao bila kujali adha wanazozipata wakulima.

Kauli hiyo imetolewa na mmoja wa wakulima wa viazi kutoka Ipelele Bw.Bakari Ngailo alipokuwa akizungumza na Green fm iliyotaka kujua adha wanazokabiliana nazo wakulima wa viazi wa eneo hilo.

Bw.Ngailo amesema eneo la soko limekuwa na changamoto kubwa kwani viazi vinapofikia hatua ya kuvunwa wakulima wengi hutegemea madalali hivyo huwapangia bei badala ya wakulima kupanga wao.

Ili kuondokana na changamoto hiyo Bw.Ngailo amewataka wakulima wa viazi katika kata ya Ipelele kuona umuhimu wa kuwa na chama chao ambacho kitawasaidia kuwa na msimamo wa pamoja kwa upande wa bei inayostahili kwa maslahi yao wenyewe.

Kwa upande mwingine Bw.Ngailo ameitupia lawama serikali na mamlaka husika kwa kushindwa kuwadhibiti wanaoendelea na utaratibu wa rumbesa ambao umekuwa ukiwanyonya wakulima kwani utaratibu huo ulipigwa marufuku na serikali lakini wahusika wamekuwa wakisafirisha viazi hivyo kwa mfumo huo na hakuna hatua zozote ambazo zimekuwa zikichukuliwa.

Maoni