WANANCHI RUHURU WAJICHANGISHA FEDHA KUJENGA ZAHANATI

WANANCHI wa Kijiji cha Ruhuru wilayani Kakonko mkoani Kigoma wamejitolea kuanza ujenzi wa Zahanati itakayogharimu zaidi ya Sh.milioni 50 kwa lengo la kutatua changamoto ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya hali inayosababisha wengi wao kupoteza maisha maisha wakiwa njiani.

Wakizungumza jana wananchi hao wakati wa ziara ya Mkuu wa Wilaya hiyo Kanali Hosea Ndagala aliyefika kukagua ujenzi wa Zahanati hiyo inayojengwa kwa nguvu za wananchi, wameiomba Serikali kuchangia jitihada hizo walizoanzisha za kujenga msingi na kuinua ukuta ili kumaliza tatizo la ukosefu wa kituo cha afya na Zahanati.

Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Ruhuru Bahati Kimpaye amesema kijiji hicho kina wakazi 2016 ambao wameanzisha ujenzi wa Zahanati hiyo baada ya kuona wanapata shida ya huduma ya afya hasa wajawazito.

Amesema usafiri mkubwa unaotumiwa na wananchi ni pikipiki ambapo kwa mama mjazito inakuwa ni changamoto huku akieleza wengine wanalazimika kutembea kwa miguu umbali wa saa tatu kufuata huduma katika vijiji vya Gwarama, Nyakayenzi na Nyanzige.

Amesema wapo baadhi ya wananchi ambao wamepoteza maisha wakiwa njiani wakifuata huduma za afya hali iliyokuwa ikiwaumiza wananchi na kuamua kuchangishana fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi huo.

Kwa upande wake Mkazi wa kijiji hicho Nesia Semagogwa amesema siku za nyuma kulikuwa na gari inafika kijiji hapo lakini sasa haipo na matokeo yake wananchi kuwa na wakati mgumu katika kupata huduma za afya.

Akizungumzia uamuzi huo, Mkuu wa Wilaya ya Kakonko Kanali Hosea Ndagala amewapongeza wananchi hao kwa kujitoa katika ujenzi huo na kuahidi yeye binafsi atatoa mifuko 20 ya saruji yeye binafsi na kuna fedha Sh.milioni 100 zimetolewa kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya ambazo zitatolewa kwa ajili ya kijiji hicho ili wamaliziea zahanati yao kwa kununua vifaa mbalimbali.

Pia Kanali Ndagala amewaagiza wananchi na viongozi wa vijiji vingine kuiga juhudi hizo na Serikali inahitaji wananchi kuwa na umiliki wa miradi kwa kuonesha juhudi zao kwenye masuala ya maendeleo.

Maoni