WANANCHI WASHUKURU SERIKALI UJENZI WA DARAJA LA MTO KILOMBERO

Wananchi wa wilaya ya Ulanga, Malinyi na Kilombero wameishuru Serikali ya Awamu ya Tano kwa kutimiza ahadi waliyoitoa kwa wananchi hao ya kuwajengea daraja la mto kilombero ambalo lilikuwa kilio chao cha muda mrefu.

Wakizungumza mbele ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa katika kijiji cha Kivukoni, mkoani Morogoro, wakazi hao wamemueleza kuwa hivi sasa changamoto zao zimetatuliwa baada ya kukamilika kwa daraja hilo.

“Tunaishukuru Serikali kwa ujenzi wa daraja hili kwani limekuwa mkombozi kwetu wananchi wa wilaya za ulanga na kilombero kwani hapo nyuma vifo vingi vimetokea pasipo kutegemewa wakati tukitumia kivuko kufuata huduma za kijamii wilaya jirani ambapo ndio kuna huduma zote za muhimu”, amesema Bi. Zainabu Mtalanga

Aidha Waziri Prof. Mbarawa ametoa wito kwa wananchi hao kulilinda daraja hilo kwa kutojihusisha na vitendo vya kuchimba kokoto chini ya daraja, kuiba alama za barabarani na kuacha kupitisha mifugo juu ya daraja kwani Serikali imetumia gharama kubwa kujenga daraja hilo na barabara unganishi katika eneo hilo.

Ameongeza kwa sasa Serikali  ipo katika hatua za kujenga kituo cha polisi katika maeneo hayo ili kimarisha ulinzi na kuhakikisha usalama unakuwepo kwa saa 24 siku saba kwa wiki.

Naye Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) mkoa wa Morogoro Mhandisi Dorothy Ntenga amemueleza Waziri Mbarawa kuwa ujenzi wa daraja hilo umejengwa kwa kuzingatia viwango vilivyowekwa kwenye mkataba na mkandarasi wa kampuni ya M/S China Railway 15 Group Corporation.

Kukamilika kwa ujenzi wa Daraja la Mto Kilombero umegharimu zaidi ya shilingi bilioni 50 ambazo zimegharamiwa na Serikali na daraja hilo litarahisisha shughuli za usafirishaji wa mazao, ufugaji na madini katika wilaya hizo na wilaya jirani.


 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (kulia), akikagua daraja la mto Kilombero lenye urefu wa mita 384 ambalo linaunganisha wilaya ya Kilombero, Ulanga na Malinyi mkoani Morogoro ambapo mpaka sasa ujenzi wake umekamilika kwa asilimia 100. Katikati ni ni Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Morogoro Mhandisi Dorothy Ntenga.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akizungumza na baadhi ya wananchi wa wilaya ya Ulanga, alipokuwa akikagua Daraja la Kilombero mkoani Morogoro.

 Muonekano wa Daraja la Kilombero lenye urefu wa mita 384 ambapo ujenzi wake umegharimiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa zaidi ya shilingi bilioni 50.Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

Maoni