ZANZIBAR YAKABIDHIWA CHETI CHA KIMATAIFA CHA UBORA WA KUTOA HUDUMA

Na Faki Mjaka-Maelezo Zanzibar 15.02.2018

Wakala wa Chakula na Dawa Zanzibar ZFDA umekabidhiwa rasmi Cheti cha mfumo wa uhakiki ubora wa huduma cha kiwango cha kimataifa cha ISO 9001:2015.

Cheti hicho cha ubora ni kielelezo cha taasisi ya ZFDA juu ya kusimamia misingi imara ya kuhakiki ubora wa huduma katika kiwango cha kimataifa.

Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa Cheti hicho Waziri wa Afya wa Zanzibar Mahmoud Thabit Kombo amesema mafanikio hayo ni matokeo ya utekelezaji wa vitendo wa azma ya serikali inayoongozwa na Dkt. Ali Mohamed Shein katika kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora za afya hususan upatikanaji chakula, dawa na Vifaa tiba.

Amesema kunahitajika ubunifu na jitihada za makusudi za kila mfanyakazi wa ZFDA kuhakikisha Chakula, Dawa, Vipodozi na Vifaa tiba ni bora na salama kwa afya za wananchi.Amefahamisha kuwa mafanikio hayo yaliyopatikana yawe chachu ya kuongeza ufanisi kiutendaji ili kufikia dira iliyowekwa.

“Mkifikia dira dira hiyo itakuwa mmetekeleza kikamilifu jukumu mllopewa na Serikali la kulinda afya ya jamii.Serikali inaaamini mnao uwezo wa kuwa taasisi bora ya udhibiti Afrika na Duniani kwani hakuna kizuizi cha kufikia dira hiyo” Alisema Waziri Kombo.Aliitaka menejimenti ya ZFDA kuimarisha udhibiti wa uingizaji wa Chakula, Dawa na Vipodozi nchini kiholela ili kulinda afya za Wazanzibari.


Waziri wa Afya Mahmoud Thabit Kombo katikati akizungumza mara baada ya kupokea Cheti cha mfumo wa uhakiki ubora wa huduma cha kiwango cha kimataifa cha ISO 9001:2015 katika hafla iliyofanyika Ofisi za ZFDA Mombasa mjini Zanzibar.

Maoni