Anaswa akisafirisha mazao bila Kulipia Mapato.


Maafisa Mapato wa Halmashauri ya wilaya ya Ngara mkoani Kagera March 24,2018 wamekamata gari likisafirisha mahindi kutoka wilayani humo kwenda mkoani Singida  bila kulipia ushuru na dereva  ametakiwa kulipia  faini ya Sh 1.67 milioni.

Afisa Mipango wa Halmashauri ya wilaya hiyo Bw.Ghalib Mkumbwa amesema gari hilo lenye namba za usajili T494 AKC lilikuwa likiendeshwa na Emanuel Kingu mkazi wa Kahama ambaye alikuwa akisafirisha magunia 389 ya mahindi kutoka Kata ya Nyakisasa na Rulenge wilayani Ngara akipita njia za panya. 

Bw.Mkumbwa  alisema gari hilo limekamatwa katika kizuizi cha barabara eneo la Kumubuga kata ya  Murusagamba, mpakani mwa wilaya ya Ngara na Biharamulo na baada ya kuhojiwa alidai ni magunia 200.

  

Bw. Mkumbwa alisema kutokana na kufungwa kwa magunia hayo Maafisa mapato walitilia mashaka  na kujiridhisha na kukuta magunia 389 yakiwa yamezidi 189 hivyo kupigwa faini na  kulipia magunia ya ziada ili kuendelea na safari yake.

Alisema baada ya kufungua na kujiridhisha   kila gunia amelipia Sh3000 na kupata Sh567,000 kisha  kumpiga faini ya Sh 500,000 ya udanganyifu na kwamba malengo ya kufanya hivyo ni kutoa fundisho kwa watu wote wanaokiuka taratibu za kulipia mapato ya serikali.


Aidha Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Ngara Erick Nkilamachumu (pichani) alisema Maafisa Biashara na Mapato wamesambazwa kila tarafa kufanya kazi ya kukusanya mapato ya ndani ili kupata fedhas za kuboresha huduma za kijamii.

Nkilamachumu amewataka wafanya biashara wa aina mbalimbali wakiwemo wa mazao kuhakikisha wanalipia mapato ya serikali kwa kukata leseni zao , kulipia majengo kwa taratibu za halmashauri hiyo vinginevyo watafikishwa mahakamani.

Maoni