Azam waipa mazoezi Serengeti Boys

Kikosi cha timu ya vijana ya Azam chini ya umri wa miaka 20 Jumamosi hii kimeipa mazoezi timu Taifa ya Tanzania chini ya umri wa miaka 17 (Serengeti Boys) katika mchezo maalumu wa kirafiki wa mazoezi uliofanyika Uwanja wa Karume, Ilala, jijini Dar es Salaam.

Katika mchezo huo ilishuhudiwa vijana wa Azam wakiibuka kidedea kwa ushindi wa bao 1-0, lililofungwa na Hamadi Aziz, dakika ya nane akitumia vema pasi ya Mahamud Said, na kudumu kwa dakika zote 90 za mchezo huo.

Serengeti Boys inayonolewa na Kocha Oscar Milambo, chini ya Mkurugenzi wa Soka la Vijana ndani ya TFF, Kim Poulsen, iliweza kuonesha upinzani mkali licha ya kufungwa bao hilo jambo ambalo linaonesha mwanga kuelekea Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Vijana wa umri huo zitakazofanyika nchini mwakani.

Kocha wa Azam Idd Aboubakar mara baada ya mchezo huo alisema kuwa ni jambo jema kuona wamecheza na timu ya Taifa na wamecheza mchezo huo wakiwa wanawaheshimu wakijua ni tunu ya Taifa.

“Kiujumla mchezo ulikuwa mzuri, tunawaheshimu Serengeti Boys, hatukuwachukulia kama ni watoto ni timu ambayo inajiandaa kimataifa, na wachezaji waliochaguliwa wanaviwango vya juu kabisa, lakini kwa upande wa timu yetu yale tuliyowaagiza na kuwaelekeza wameyafanyia kazi na tumebahatika kupata ushindi,” amesema Aboubakar.

Maandalizi ya AFCON U17

Mechi hiyo ilikuwa ni maalumu kwa ajili ya kuwapa mechi ya ushindani vijana hao wa Serengeti Boys, ambao wanaendelea na programu kali ya mazoezi kuelekea fainali hizo.

Maoni