KUSHINDWA KULINDA NA KUTETEA MASLAHI YA TAIFA, KWA KIJANA NI MATOKEO YA KUKOSA UZALENDO NA UTII- NDG. NGEMELA LUBINGA.

 Jamii yoyote duniani inaoutaratibu wa kuandaa watu wake kwa kusudi kubwa la kuweza kulinda na kutetea maslahi ya kundi/mazingira au Taifa husika. Maandalizi na utamaduni huu huwa na sura inayolingana na hitajio la muda huo katika jamii.

Haya yamesemwa na Ndg. Ngemela Lubinga Katibu wa NEC Siasa na Uhusiano wa Kimataifa (SUKI)- CCM jioni leo 03/03/2018 alipokuwa akitoa mada ya "Intelijensia na Ulinzi Ndani na Nje ya CCM" iliyoandaliwa na Umoja wa Vijana wa CCM kwa lengo la kuwajengea uwezo na kuwakumbusha viongozi wake majukumu mbalimbali ya Chama.

Akiendelea kutoa ufafanuzi juu ya mada husika Ndg Lubinga alisema, Intelijensia  ni uwezo wa kupata taarifa zozote zinazomuhusu mtu mwenyewe na mazingira yake ya marafiki na maadui na kuhakikisha kwamba analinda usalama wa vitu alivyokabidhiwa au anavyovilinda. Kushindwa kulinda Taifa ni matokeo ya kukosa uzalendo, utii, uadilifu na usikivu mambo ambayo hupelekea kuibuka kwa ubinafsi, vitendo vya rushwa, hujuma na ugaidi. 

Hivyo ili tudumu kwa muda mrefu kwenye mfumo pindi tunapopewa dhamana za kiuongozi ni lazima turidhike na tulivyonavyo, tuheshimu wanaotupa dhamana hizo, tujitoe kwa ajili ya Taifa letu, tuwe wasiri, tupende kusikiliza, tuwe wachujaji wa maneno ya kuongea na tujifunze kuishi kimkakati kwa kuwa makini na watulivu. Alisema.

Ndg. Lubinga alimalizia kwa kuwakumbusha viongozi wote kutambua wanachopaswa kusimamia katika dhamana zao, kulinda nchi na kuwa wazalendo kwa Taifa na Chama kwa ujumla.

Kambi ya Vijana katika Mkoa wa Dar Es Salaam lilianza rasmi tarehe 02/03/2018 na kutarajiwa kumalizika tarehe 05/03/2018 katika Chuo Cha Mwalimu Nyerere. Viongozi wasiopungua 200 wanaotokana na Kamati za Utekelezaji za UVCCM kutoka wilaya 5 za mkoa huo wamehudhuria kambi hilo.

IMETOLEWA NA 
IDARA YA SIASA NA UHUSIANO WA KIMATAIFA (SUKI)
CHAMA CHA MAPINDUZI
03/03/2018

Maoni