MASHINDANO NDONDO CUP YAZINDULIWA RASMI


MASHINDANO ya Ligi ya Ndondo CUF kwa mwaka 2018 yanatarajiwa kufanyika kwenye mikoa kadhaa nchini na tayari yamezindulwa rasmi leo huku ikielezwa maandalizi na fedha ambazo zitapatikana kwa kila timu kutokana na hatua ambayo itakuwa inafikia.

Akizungumza leo katika Viwanja vya Escape 1 Mikocheni jijini, Mwenyekiti wa Maandalizi ya mashindano hayo Shafii Dauda amesema mchakato wa usajili katika Mkoa wa Dar es Salaam utaanza leo kupitia usimamizi wa Chama cha Soka Mkoa(DRFA) na ada ya usajili ni Sh.300,000 zitakazolipwa kupitia akaunti ya chama hicho.

Ametaja mikoa mingine ambayo mashindano hayo yatafanyika ni Mwanza na Ruvuma na kufafanua kuwa Mkoa wa Dar es Salaam utafungua mashindano hayo Aprili 4 mpaka Mei 6  mwaka huu.

"Na baada ya kupatikana kwa timu 32 kutoka kwenye hatua za awali yatapangwa rasmi makundi kwa timu zitakazoshiriki na zitaanza kumenyana kwenye Uwanja wa Bandari na Kinesi jijini Dar es Salaam kuanzia Juni 1 mpaka Julai 22 mwaka huu,"amesema.

Dauda amesema mshindi wa kwanza katika Mkoa wa Dar es Salaam atapata kitita cha Sh.milioni 10, Mshindi wa pili Sh.milioni 5, Mshindi wa 3 atapata  Sh.milioni  3 na Mshindi wa nne atapata Sh.milioni 1.

"Mbali na kitita cha fedha kwa mshindi wa kwanza hadi mshindi wa nne timu zote zitakazoingia kwenye hatua ya 16 bora zitapewa Sh.500,000 kwa kila timu kwa ajili ya maandalizi.Pia zitakuwa zikipewa usafiri kwa kuwachukua kuwapeleka uwanjani na kuwarudisha majumbani.Kila siku ya mechi watapa chakula cha mchana.

"Kwa timu zitakazoingia hatua ya nane bora zitapewa Sh.milioni 1 kwa kila timu kwa ajili ya maandalizi na timu zitakazoingia hatua ya nne bora zitapewa Sh.milioni 1.5 za maandalizi.Kwa timu ambazo zitaingia hatua ya fainali zitapewa Sh.milioni 2 za maandalizi,"amesema Dauda.

Mwenyekiti wa kamati ya Ndondo Cup, Shafii Dauda akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya michuano ya Ndondo Cup itayoanza kutifuana Mwezi ujao mwaka huu leo katika fukwe za  Escape 1 Mikocheni Jijini Dar es Salaam.

Maoni