MBUNGE AZINDUA MRADI USAMBAZAJI MBEGU ZA VIAZI LISHE

Na Allan Ntana, Urambo

MBUNGE wa jimbo la Urambo Mkoani Tabora Magreth Sitta amezindua mradi wa ugawaji na usambazaji mbegu za zao la viazi lishe linalosimamiwa na Mradi wa ‘Sambaza Marando Fasta’ wilayani humo.

Akikabidhi mbegu hizo jana Sitta alisema mradi huo unaoratibiwa na Shirika la ANSAF la jijini Dar es salaam ni muhimu sana kwa sababu ya urahisi wake na manufaa makubwa watakayopata wananchi kwa kuzalisha zao la viazi lishe.Alisema semina iliyotolewa na Shirika hilo bungeni mjini Dodoma ilimhamasisha kuleta mradi huo kwa wananchi wake jimboni na mwezi Desemba mwaka jana alianzisha shamba la zao hilo lenye ukubwa wa ekari 2 ili kuzalisha mbegu hizo.

‘Nawashukuru sana ANSAF na Kituo cha Utafiti wa Mazao Ukiriguru kwa kufanikisha mradi huu hapa Urambo, sasa mbegu zipo tayari na leo tunazigawa bure kwa vikundi vya wakulima wa kata zote 18 jimboni kwangu’, alisema.Alisema atahakikisha mbegu hizo zinazalishwa kwa wingi na kusambazwa katika vijiji vyote jimboni kwake na wilayani nyingine za mkoa huo ili zao la viazi lizalishwa kwa wingi sana katika mkoa huo ili kumwinua kiuchumi mwananchi.

Afisa Mtafiti kutoka Kituo cha Utafiti cha Ukiriguru cha jijini Mwanza Rahila Amour aliwataka wananchi wa mkoa huo na mikoa jirani kuchangamkia mradi huo kwa kuwa una faida nyingi na mbegu zinapatikana kwa urahisi mno, alibainisha mbegu zilizopo kuwa ni Kabode, Kakamega na Mataya.Alisema Mradi huo unafadhiriwa na Shirika la Bill and Melinda Gates Foundation la nchini Marekani kwa kushirikiana na Taasisi ya ANSAF ya jijini DSM, Wizara ya Kilimo na Chakula na Kituo cha Utafiti wa Mazao cha Ukiriguru-Mwanza.

Mtafiti Mwenza kutoka Kituo cha Ukiriguru Eric Chang’a alisema zao la viazi ni muhimu sana kwa sababu ni lishe nzuri (chakula), linaongeza mapato na ni kinga dhidi ya upofu, hivyo akawataka wananchi wengi zaidi kuchukua mbegu hizo.Alisema mbegu hiyo imefanyiwa utafiti wa kina na Wataalamu wa Ukiriguru na kujiridhisha kuwa ni mbegu bora inayopaswa kulimwa na wakulima wote hapa nchini kwa kuwa inachukua muda mfupi sana takribani miezi 3-4kutoa viazi.

Baadhi ya Madiwani waliokuwepo katika tukio hilo Elizabet Mkwenda na Blandina Magupa walimpongeza mbunge wao kwa kuleta mradi huo na kuamua kuzalisha mbegu na kuzigawa bure kwa wananchi wake.Shughuli ya uzinduzi wa Mradi huo ilihudhuriwa na Mkurugenzi wa Kanda wa Kituo cha Utafiti Ukirigiru Dr Everine Lukonge, Meneja wa TRA Mkoa wa Tabora, Wataalamu Watafiti kutoka Ukiriguru, Katibu Mwenezi wa CCM Mkoa na mwenzake wa wilaya na viongozi wa UWT wilaya.

Mbunge wa Jimbo la Urambo Magreth Sitta (aliyesimama katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Vikundi wa Wakulima kutoka kata 18 za wilaya hiyo baada ya kuwakabidhi mbegu za viazi ili wakazismabaze. Picha na Allan K.

Maoni