MBUNGE CHATANDA ATAKA UKAGUZI TSH. MILIONI 230, UJENZI SHULE YA JOEL BENDERA SEC

Mbunge wa Jimbo la Korogwe Mjini mkoani Tanga Mary Chatanda amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Korogwe Jumanne Shauri kupeleka wakaguzi kwenye Shule ya Sekondari Joel Bendera iliyopo Kijiji cha Kwakombo, Kata ya Kwamsisi.

Ni kutaka kubaini ukweli kuhusu matumizi ya fedha baada ya sh. milioni 150 zilizopelekwa shuleni hapo kumalizika, kabla ya ujenzi wa mabweni mawili kumalizika, huku tena zikihitajika sh. milioni 17 kumalizia ujenzi huo.

Chatanda alibaini hilo baada ya Machi 3, 2018 kufanya ziara kata ya Kwamsisi, na kusomewa taarifa na Mkuu wa Shule hiyo Nasson Msemwa kudai sh. milioni 150 zilizotolewa na Serikali kwa ajili ya kujenga mabweni hayo ikiwa ni pamoja na kuweka samani, fedha zake zimekwisha.

“Mheshimiwa Mbunge, Serikali ilituletea sh. milioni 230, ambapo sh. milioni 150 kwa ajili ya ujenzi wa mabweni mawili ya wasichana na wavulana na sh. milioni 80 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa mapya manne. Fedha kwa ajili ya ujenzi wa mabweni ambapo tupo kwenye hatua za mwisho zimekwisha. Na ili tukamilishe mabweni hayo kunahitajika sh. milioni 17.

“Kwa upande wa ujenzi wa madarasa manne, bado tunakwenda vizuri, kwani pamoja na ujenzi kuwa kwenye hatua za mwisho, bado tuna sh. milioni 28” alisema Msemwa.

Mbunge wa Korogwe Mjini Mary Chatanda (wa tatu kulia) akisikiliza taarifa inayosomwa na Mkuu wa Shule ya Sekondari Joel Bendera Nasson Msemwa (wa pili kushoto). Hapo ndipo Chatanda aliliamsha ‘dude’ kutaka kujua kwa nini sh. milioni 150 zimeshindwa kukamilisha mabweni mawili.Yussuph Mussa, Korogwe

Madarasa mapya manne ya Shule ya Sekondari Joel Bendera, Kijiji cha Kwakombo, Kata ya Kwamsisi, Halmashauri ya Mji Korogwe. Madarasa hayo ambayo yapo kwenye hatua za mwisho kukamilika, Serikali ilitenga sh. milioni 80 kujenga madarasa hayo. (Picha na Yusuph Mussa).

Moja ya mabweni yaliyopo Shule ya Sekondari Joel Bendera Kijiji cha Kwakombo, Kata ya Kwamsisi, Halmashauri ya Mji Korogwe. Mabweni mawili yaliyojengwa shule hiyo, kila moja litakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 80 kwa wakati mmoja.PICHA ZOTE NA YUSSUPH MUSSA.

Maoni