MWENYEKITI UWT AMZUNGUMZIA MWANAFUNZI CHUO KIKUU DAR ANAYEDAI AMETEKWA


*Amtaka aache kutafuta kiki kwa staili hiyo,awapa somo vijana wa kitanzania

Na Said Mwishehe,Globu ya Jamii

MWENYEKITI wa Jumuiya ya Wanawake Tanzania(UWT) Gaudentia Kabaka amewataka vijana wote nchini kuacha tabia ya kuichafua Serikali kwa kujifanya wanatekwa kwani madhara yake ni makubwa.

Amesema vijana wa kitanzania wanatakiwa kusoma kwa bidii ili waweze kuisaidia nchi yao katika kuleta maendeleo badala ya kutafuta kiki za kitoto.

Kabaka ametoa kauli hiyo alipokuwa anazungumzia madai ya mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Abdul Nondo ambaye alitoa taarifa kudai ametekwa na kisha kwenda kutelekezwa mkoani Iringa.

Hata hivyo wakati mwanafunzi huyo akitangaza kutekwa wapo baadhi ya watu waliosafiri naye kutoka Dar es Salaam hadi Iringa kwa kutumia basi la New Force wameelezea namna alivyokuwa amesafiri kwa kujificha ficha uso kwa kujifunika na shuka la kimasai.

Hivyo Kabaka akizungumzia madai ya mwanafunzi huyo amesema ni kitendo kibaya sana mwanafunzi kudai ametekwa wakati anajua anachokifanya na inaonesha hakuwa na nia njema na Serikali.Amesema kuwa amefuatilia taarifa mbalimbali zinazomhusu Nondo na kwa sehemu kubwa zinaonesha alichokifanya ni kutafuta kiki bila kujua madhara yake na anataka kuuaminisha umma kuwa ametekwa na Serikali.Kabaka amemzungumzia hayo baada ya waandishi wa habari kutaka kupata kauli ya UWT kuhusu kitendo alichofanya mwanafunzi huyo na wao kama wazazi wanalichukuliaje.

Hivyo akasema kama wanawake wa Tanzania ambao pia ni wazazi,walezi na wakati mwingine ndio bibi wamesikitishwa na madai ya kijana huyo."Kwanza najaribu kuangalia baada ya kutangaza ametekwa wazazi wake walikuwa kwenye hali gani.Kwa vyovyote walikuwa katika wakati mgumu na hata mimi binafsi niliumia maana najua uchungu wa mtoto.

" Alichokifanya ni kutafuta kiki vijana wa siku hizi kama mbavyo mnasema wenyewe.Kwetu sisi UWT tunaamini kijana anayetaka kutafuta kiki yenye heshima ni kusoma kwa bidii na akihitimu masomo yake awe msaada kwa nchi katika kuleta maendeleo,"amesema.Kabaka amesema vijana ni wakati wa kutambua taifa linawategemea katika kuleta maendeleo hivyo badala ya kujikita kwenye mambo yasiyo na tija wakawekeza nguvu zao katika kusaidia nchi kusonga mbele kimaendeleo.

Maoni