MAMLAKA ya Vitambulisho vya Taifa(NIDA) inatarajia kuzindua usajili na utoaji wa vitambulisho hivyo katika mikoa mitatu ya Katavi, Kigoma na Rukwa.
Pia NIDA kwa kushirikiana na Wizara ya Madini , imeanza kuwasajili watu wote watakaoishi, kufanya kazi au biashara ndani ya eneo lililozungushiwa ukuta lenye madini ya TANZANITE huko Mererani mkoani Arusha.
Akizungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam, leo, Kaimu Ofisa Uhusiano wa NIDA, Rose Joseph, alisema mpaka sasa mamlaka hiyo imaendelea na usajili na utoaji vitambulisho vya uraia katika mikoa 20.
“Hivi karibuni tutafanya uzinduzi katika mikoa mitatu iliyobaki ambayo ni Kigoma, Rukwa na Katavi . Wananchi katika mikoa hii watakuwa na muda wa miezi mitatu wa kujisajili, na hivyo tutakuwa tumeifikia nchi nzima,”alisema Rose.Ofisa huyo alisema pia NIDA taangu Novemba mwaka uliopita ilianza usajili wa mkupuo katika mikoa mbalimbali na muda ulikuwa ukiongezwa kadri ilivyokuwa uinaruhusu.
“Tayari baadhi ya mikoa imemaliza kazi ya kusajili kwa mkupuo ikiwemo mikoa ya Mara na Iringa,”.alieleza Rose.Alisema katika kazi hiyo ya usajili NIDA kwa kushirikiana na Idara ya Uhamiaji wanapeleka maofisa hadi ngazi ya kata na vijiji, ili kuhakikisha kazi hiyo inakwenda kwa mchujo sahihi na wale wote wanaosajiliwa wawe na sifa na vigezo kuwa raia wa Tanzania. “Tunasajili vitambulisho vya aina tatu ambavyo ni vya uraia, mkimbizi na mgeni na kumekuwa na ufanisi mkubwa,”alifafanua ofisa uhusiano huyo.
Kaimu Ofisa Uhusiano Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) Rose Joseph akielezea mikakati ya kuzindua usajili wa vitambulisho Kigoma, Rukwa na Katavi sambamba na ndani ya mgodi wa Tanzanite.
Maoni
Chapisha Maoni