MWANAFUNZI KUDAIWA KUCHOMA MOTO BWENI LA WAVULANA MANG'OTO SEKONDARI

MKUU wa shule ya sekondari Mang’oto wilayani Makete mkoani Njombe Bonaventure Mgaya amezitaja mali zilizoteketea kwa moto katika bweni la wavulana shuleni hapo pamoja na makisio ya gharama hizo.

Akizungumza na Green FM jana kujua kinachoendelea shuleni hapo baada ya kuripotiwa kuungua kwa bweni hilo usiku wa wa kuamkia Machi 13, Mwalimu Mgaya amesema wanafunzi wote 142 wanaokaa katika bweni hilo walitoka salama


Mgaya amezitaja mali zote za shule pamoja na za wanafunzi zilizoungua na jengo hilo limeteketea kabisa hali itakayolazimu kujenga upya.
Aidha amesema walimu shuleni hapo walitoa utaratibu kwa kujua thamani ya vitu vyote vilivyoungua ambapo walitoa karatasi kwa wanafunzi ili kujua thamani ya vitu vya wanafunzi walivyounguliwa
Amesema baada ya utaratibu huo walifanya tathimini ya awali ambayo ilionesha mali za wanafunzi, jengo la shule pamoja na mali za shule zilizokuwemo ndani ya jengo hilo kukadiriwa kufika milioni mia moja na ishirini na laki saba.

Kwa upande wake kaimu mkuu wa wilaya ya Makete ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Wanging’ombe Comred Ally Kasinge amesema Amefurahishwa na hatua za awali zilizochukuliwa na kumtaka mkuu wa shule kuhakikisha anafanya tathimini halisi ya mali zilizoungua haraka pasipo kukadiria.
Pia amemtaka mkuu wa shule kukaa na bodi ya shule ili kuona namna ya kukabiliana na tatizo hilo huku akisisitiza kutowatwisha mzigo wazazi pekee katika jambo hilo.
Kasinge ameunda kamati katika tatizo hilo na ameagiza kuwa ndani ya siku tatu ipate majibu ya msingi ya kuona namna ya kukabiliana na jambo hilo na kuwaepusha wanafunzi na adha waliyonayo katika kipindi hiki.


Bweni la wanafunzi wavulana katika shule ya sekondari Mang’oto liliungua majira ya saa mbili usiku wa kuamkia leo, huku chanzo kikielezwa kuwa ni kuchomwa na mwanafunzi wa kidato cha pili Essau Aldo Msigwa akiwa na lengo la kuwakomoa wanafunzi wenzie waliokuwa wakimtuhumu kwa wizi shuleni hapo ambapo alichukua magodoro ya wanafunzi hao wanne na kuyachoma ndani ya bweni hilo hatimaye jengo zima likaungua.
Siku moja kabla ya kuchoma bweni hilo mtuhumiwa huyo alikuwa anatuhumiwa kubomoa na kuiba Bidhaa katika kibanda cha mmoja wa walimu shuleni hapo.
Kwa mujibu wa maelezo ya mkuu wa shule kupitia barua aliyoiandika mwanafunzi Essau amesema mwanafunzi huyo alikiri Kufanya makosa hayo ikiwemo la kuchoma bweni hilo.
Mwanafunzi huyo amechukuliwa na vyombo vya ulinzi na usalama ili kukamilisha hatua zaidi za kisheria za tukio hilo. 

Chanzo: Green fm. 

Maoni