UNILIFE CAMPUS PROGRAM YAZINDULIWA KWA KISHINDO JIJINI DAR ES SALAAM

 Mhe Esther Michael Mmasi, Mbunge anaewakilisha vyuo vikuu nchini katika Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania March 16,2018 amezindua rasmi programu maalumu inayohusu maisha ya wanafunzi vyuoni (University Life Campus) maarufu kama UNILIFE CAMPUS

Uzinduzi huo uliofanyika katika Viwanja vya Chuo cha Elimu ya Biashara CBE, umeongozwa na Naibu Waziri wa Elimu nchini Mhe William Olenasha alieongozana na viongozi mbali mbali wa kitaifa akiwemo Waziri wa mambo ya ndani, Mhe Lameck Mwigulu Nchemba

Mhe Esther Mmasi alisisitiza kwamba programu hii itazidi kuwajengea uwezo wanafunzi wa vyuo katika Elimu ya kujitambua na kujiamini ikiwemo kutumia Elimu yao kutambua Fursa mbali mbali zinazowanguka 

Mhe William Olenasha aliwasisitiza wanafunzi kuendelea kutumia Maktaba na kusisitiza kwamba mitandao (google) ina nafasi yake lakini haiwezi kuchukua nafasi ya maktaba. Mhe aliongezea kwamba katika mitandao kuna Habari za kweli na Habari za kupotosha hivyo inahitaji umakini mkubwa Zaidi katika kuchambua Habari au taarifa za mitandaoni.

Katika maoni yake kwa wanafunzi Mhe Mwigulu Nchemba ambae ni Waziri wa Mambo ya ndani amewasisitiza wanazuoni kwamba historia ya maisha ya nyuma isiwakatishe tamaa kufikia malengo yao, Mhe Mwigulu amesema wanafunzi wajitokeze kuomba nafasi mbali mbali za ufadhili (scholarships) ambazo zinakuja kwa nchi za Afrika, amewasihi wanazuoni kuhakikisha wanatumia Elimu yao kutoa ushauri wa kitaalamu kwa Serikali badala ya kushabikia bila kufanya tafiti na kujikuta wanaingia kwenye mkondo wa kulichafua Taifa 


Uzinduzi wa Unilife Campus umewakutanisha wanazuoni kutoka vyuo mbali mbali ndani ya Mkoa wa Dar es salaam.

Shirika la NSSF kama mdhamini Mkuu wa programu hii, kupitia muwakilishi wake amewasisitiza wanafunzi kujiunga na mpango wa Afya na Akiba yaani AA+. Huu ni mpango wa Bima ya afya ambayo inatolewa sawa na bure, na kama mwanafunzi akijiunga na Rafiki zake wa karibu wanapata nafasi ya kutibiwa bure pia.

Katika kuhitimisha Mhe Esther Michael Mmasi (Mb) alisema programu hiyo itazunguka vyuo vyote nchini na kwa awamu ya kwanza watatembelea vyuo vya CBE, IFM, KIU, ST. JOSEPH, ARDHI, TIA, MUHAS, MWENGE UNIVERSITY, MOSHI COOPERATIVE pamoja na KCMC

Mkuu wa Chuo cha CBE Professor Mjema alitoa Maneno ya shukrani kwa chuo chake kuwa cha kwanza kutembelewa na programu hii, alisisitiza kwamba CBE ambacho pia ndio Chuo Bora cha Mwaka 2017 (College of the Year) bado kipo makini kuhakikisha wanazalisha wanafunzi wenye taaluma na ujuzi unaotakiwa na waajiri.


Uzinduzi huu wa Unilife Campus umeamsha shauku kubwa ya mafanikio kwa wanazuoni kutumia taaluma yao katika kujenga maisha yao na Taifa kwa ujumla.

Maoni