ZIARA YA KUKAGUA NA KUFUATILIA ILANI YA UCHAGUZI YA CCM MWAKA 2015 – 2020 WILAYA LA KILOSA MKOA WA MOROGORO

22 March 2018

Akiwa Wilayani Kilosa Jimbo la Mikumi Mkoa wa Morogoro Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi Ndg. Humphrey Polepole ameanza ziara ya Kata kwa Kata, Kijiji kwa Kijiji, Kaya kwa Kaya ya kukagua na kufutilia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM Mwaka 2015 – 2020. 

Katika ziara yake Ndg. Polepole ametembelea kata ya Mabwerebwere Kijiji cha Mamoyo na amepokea kilio cha wananchi kuhusu ubovu wa barabara na Migogoro ya Ardhi ambapo amewahakikishia kuwa CCM imekwisha ielekeza Serikali katika mwaka ujao wa fedha 2018/2019 kuanza ukarabati na ujenzi wa barabara ya Kilosa Mjini kupitia Mamoyo kuelekea Kimamba, 

na kuhusu migogoro ya Ardha hususani kijiji cha Kondoa Ndg. Polepole amemuelekeza Ndg. Adam Mgoyi Mkuu wa Wilaya ya Kilosa kwenda kwenye maeneo hayo na kuwasikiliza wananchi ili kuyapatia ufumbuzi wa kudumu matatizo hayo ya migogoro ya ardhi.
 
“Tunataka Viongozi wanaoshughulika na shida za watu, Mkuu wa Wilaya uende kwenye maeneo yanayo lalamikiwa ili kuhakiki eneo kwa eneo ili kumaliza matatizo ya ardhi”. amesisitiza Ndg. Polepole

Ziara ya ndg. Polepole imemfikisha hadi Kata ya Tindiga ambayo ziara hiyo imekuwa ni muarubaini wa tatizo la maji kwa wananchi wa kata hiyo ambapo ameielekeza Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa kutafuta na kupeleka Tshs. Milioni 61 kwenye Kata ya Tindiga kwaajili ya ujenzi wa miundo mbinu ya maji ili wananchi wapatiwe maji safi na salama kwa urahisi na uhakika.

Wakati uo huo Ndg. Polepole amekutana na wanufaika wa mpango wa Serikali ya CCM wa kunusuru Kaya Maskini (TASAF) katika Kata ya Mikumi Kijiji cha Ihombwe na kisha kukagua mradi mkubwa wa Maji katika kata ya Mikumi ambapo ameendelea kusisitiza kuwa Serikali ya CCM itafanya uhakiki wa wanufaika wa TASAF ili wanaostahili pekee ndio wanufaike na amewataka wananchi wa Kata ya Mikumi kuutunza vizuri mradi wa maji kwa sababu Serikali ya CCM imetumia fedha nyingi za wananchi kuwekeza kwenye mradi huo.

Akiwa katika eneo la mradi wa maji kata ya Mikumi Ndg. Polepole akawaasa wana CCM kukabiliana na upotoshwaji juu ya ni nani aliyeleta mradi wa maji na kwamba mradi wa maji Mikumi  ni maelekezo ya Sera za CCM kwa Serikali na ni sehemu ya ahadi za CCM zilizoko katika Ilani ya Uchaguzi ya Mwaka 2015-2020.

Aidha Ndg. Polepole ametembelea katika Kata ya Ruaha katika Kijiji cha Ruaha ambapo amekagua Kivuko cha waenda kwa miguu ambacho kimejengwa kama sehemu ya Mpango wa kunusuru kaya masikini (TASAF).

Akiwa katika kukagua kivuko hicho mamia ya wananchi wakamtaka Ndg. Polepole asiishie kukagua kivuko tu bali asikilize na kero zao na kwamba Uongozi wa Kijiji na Kata umekuwa ukitoa maendeleo kwa ubaguzi na hasa dhidi ya wanachama wa CCM. Wananchi wakaendelea kusema hata Mpango wa TASAF walengwa walipangwa kwa upendeleo wa uchama na kuwabagua wananchi walio onekana ni wana CCM.

Ndg. Polepole akamuagiza Afisa wa TASAF Mkoa wa Morogoro na Afisa wake wa Wilaya ya Mikumi kurejea kijiji cha Mikumi Wiki ya kwanza ya Mwezi wa Nne ili kuhakiki wanufaika hao, na kuhusu Mwenyekiti huyo ambaye pia kwa miaka mitatu hasomi mapato na matumizi akamuelekeza Mkuu wa Wilaya kufika katika kijiji cha Ruaha ili kwa mujibu wa Sheria na Kanuni kuchukua hatua stahiki kwa Mwenyekiti huyo ambaye pia ndiye Diwani wa Kata ya Ruaha.

Katika Kijiji cha Kifinga Polepole ameshiriki ujenzi wa kituo cha afya cha kata ya Ruaha na amewaeleza wananchi kwamba CCM ndio Chama chenye dhamira ya dhati ya kuwaletea maendeleo na akatumia fursa hiyo kuwajulisha wananchi kuwa CCM imekwisha ielekeza Serikali kupeleka Tshs. Millioni 200 kwaajili ya ununuzi wa vifaa tiba pindi tu ujenzi wa Kituo hicho cha afya cha kata ya Ruaha ujenzi wake utakapo kamilika.  

“CCM ndio chama pekee chenye uwezo wa kusema tenda na likatokea, ukitoa Shilingi Milioni 400 zilizotengwa ili kukamilisha ujenzi, tayari Chama tumeelekeza kuongezwa kwa Tshs. Milioni 200 kwaajili ya ununuzi wa vifaa tiba pindi tu ujenzi utakapokamilika” amesema Ndg. Polepole

Huu ni muendelezo wa ziara za Chama Cha Mapinduzi (CCM) za kukagua na kufuatilia utolewaji wa maendeleo kwa wananchi na utatuzi wa changamoto za wananchi ikiwa nikutafsiri kwa vitendo dhana ya chama cha watu na kinachoshughulika na shida za watu.

Imetolewa na,
IDARA YA ITIKADI NA UENEZI
CHAMA CHA MAPINDUZI (CCM)

Maoni