Ajali Dsm,Mabasi yaendayo haraka kugongana na pikipiki maarufu kama bodaboda.

Mabasi yaendayo haraka yanayotoa huduma jijini Dar es Salaam yameendelea kukumbwa na matukio ya ajali, baada ya basi moja lililokuwa likitokea Gerezani kuelekea Kimara kupata ajali ya kugongana na pikipiki maarufu kama bodaboda, katika eneo la Shekilango.

Ajali hiyo iliyotokea majira ya saa sita mchana, ilisababishwa na boda boda iliyokatisha ghafla katika eneo la taa za kuongezea magari eneo hilo la Shekilango, ambapo dereva wa Mwendokasi katika juhudi za kumkwepa, aliparamia moja ya milingoti ya taa hizo na kusababisha uharibifu mkubwa.

Dereva wa bodaboda ambaye alijeruhiwa vibaya na kukimbizwa hospitali kwa msaada wa wasamaria, hakutambuliwa jina wala makazi yake kwa mara moja, lakini pikipiki aliyokuwa akiendesha imesajiliwa kwa nambari MC 215 BKM, ambapo wakati akipata ajali hiyo alikuwa na abiria wakitokea upande wa Ubungo kuelekea Sinza.

Mashuhuda wa ajali hiyo wamesema hiyo si ajali ya kwanza kutokea katika eneo hilo kukusisha mabasi ya mwendokasi, huku wakiwalaumu madereva wa vyomvo vingine vya moto kuingilia njia ya mabasi hayo, lakini pia kutofanya kazi kwa taa za barabarani wakati mwingine, ni chanzo cha kutokea ajali hizo.

Hakuna madhara yaliyotokea kwa upande wa abiria waliokuwa kwenye basi, ingawa basi lenyewe na pikipiki vimearibika vibaya.

Maoni