ASFC: Singida United waangusha mbuyu, watinga nusu fainali

Timu ya soka ya Singida United kwa mara ya kwanza imefanikiwa kufuzu katika hatua ya nusu fainali ya michuano ya Azam Sports Federations Cup baada ya kuwafunga mabingwa wa zamani Dar Young Africans kwa mikwaju ya penati 4-2 baada ya dakika 90 kumalizika kwa sare ya 1-1.

Mchezo huo wa mwisho wa robo fainali umefanyika katika uwanja wa Namfua mjini Singida na kushuhudiwa kwa mara nyingine timu hizo zikitoka sare nyingine baada ya mchezo wa ligi mwaka uliopita kutoka sare ya 0-0.

Yanga ndio waliokuwa wa kwanza kupata bao katika dakika ya 23 ya kipindi cha pili kupitia kwa kinda Yusuf Mhilu baada ya kuonganisha kwa kichwa mpira wa kona uliochongwa na Ibrahim Ajib.

Wakati Singida United wao walipata bao la kusawazisha dakika mbili tu baada kuanza kwa kipindi cha pili kupitia kwa Kenny Ally Mwambungu ambaye alipokea pasi ya bao kutoka kwa Mudathiri Yahaya na kumchambua kipa Youthe Rostand ambaye alishindwa cha kufanya.

Mpaka dakika 90 zinamalizika kwa amri ya saa ya mwamuzi Hance Mabena, Singida United ambao walikuwa wenyeji wa mchezo huo walikuwa na bao moja na Yanga nao walikuwa na bao moja, hivyo kwa mujibu wa kanuni mapigo ya penati yalitumika kuamua mshindi.

Mikwaju ya penati

Penati za wenyeji Singida United zilifungwa na Shafik Batambuze, Tafadzwa Kutinyu, Kenny Ally Mwambungu na Elinyesia Sumbi huku Maliki Antir akikosa penati yake.

Wakati penati za Yanga zikifungwa na Kelvin Patrick Yondani na Gadiel Michael Mbaga, Huku Pappy Kabamba Tshishimbi na Emmanuel Martin wakikosa penati zao

Singida United imeungana na Mtibwa Sugar, JKT Tanzania na Stand United kucheza katika hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo na atacheza na JKT Tanzania katika mchezo huo.

Vikosi vilivyocheza.

Singida United: Ally Mustapha, Michelle Rusheshangoga, Shafiki Batambuze, Kennedy Juma, Malik Antiri, Mudathir Yahya, Nizar Khalifan, Kenny Ally, Lubinda Mundia, Tafadzwa Kutinyu na Kiggi Makasy/Elinyesia Sumbi.

Akiba: Said Lubawa, Miraji Adam, Rolland Msonjo, Salumu Chuku, Yusuph Kagoma na Elinyesia Sumbi.

Yanga SC: Youthe Rostand,  Juma Abdul, Gadiel Michael, Andrew Vicent, Kelvin Yondani (C), Said Juma Makapu/Emmanue Martin, Yussufu Mhilu, Pappy Kabamba Tshishimbi, Obrey Chirwa, Pius Buswita na Ibrahim Ajib.

Akiba: Ramadhan Kabwili, Hassan Ramadhan Kessy, Mwinyi Haji, Abdallah Shaibu, Raphael Daud, Juma Mahadhi na Emmanuel Martin.

Maoni