HALMASHAURI KIGAMBONI KUFUNGUA KIDATO CHA TANO,SITA JULAI MWAKA HUU

Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni inatarajia kufungua kidato cha tano na sita Julai mwaka huu katika Shule ya Sekondari Nguva kwa kuwa na wanafunzi 160 wa kiume pekee ikiwa na michepuo ya PCM,PCB,HGE na EGM. 

Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigamboni Bw.Stephen Katemba amesema kuwa katika kutatua changamoto ya ukosefu wa Shule ya Sekondari yenye kidato cha tano na sita kwenye Halmashauri, na kutimiza maelekezo ya Serikali kwa kila Halmashauri kuwa na shule ya kidato cha tano na sita, Manispaa iliamua kuboresha miundombinu ya Shule ya Nguva ili iweze kukidhi mahitaji hayo. 

Aidha amesema kuwa mradi huu unatekelezwa kwa thamani ya shilingi 492,864,576 kwa kushirikiana na Serikali kuu, ambapo Serikali kuu imeweza kuchangia kiasi cha shilingi 259,000,000 na vyanzo vya ndani vya Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni ilichangia shilingi 233,864.576. 

Mkurugenzi amesema kwamba ili kuhakikisha Shule ina hadhi ya kidato cha tano na sita kwa mujibu wa vigezo vya wizara, ujenzi wa mabweni mawili kwaajili ya wanafunzi, vyoo, ujenzi wa daharia ambao bado unaendelea, ujenzi wa madarasa manne na ununuzi wa madawati, ununuzi wa vitanda kwaajili ya mabweni ya wanafunzi, ukarabati wa maabara ya sayansi na ujenzi wa jengo la utawala linalojengwa kwa juhudi za Mkuu wa Mkoa Mh. Paul Makonda vimefanyika . 

 Muonekano wa ubavuni wa jengo la bweni la wanafunzi  

  moja ya chumba cha wanafunzi ndani ya bweni  ​

 korido la moja ya bweni litakalotumiwa na wanafunzi wa kidato cha tano

 ujenzi wa jengo la utawala ukiendelea

moja ya jengo la maabara ya kisayansi.

Maoni