MD KAYOMBO AREJESHA VIBANDA 204 CHINI YA MANISPAA YA UBUNGO

Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo ndg. John Lipesi Kayombo kwa mara nyingine tena amefanya ziara katika kata ya Sinza eneo la Sinza Makaburini na kufanya mkutano na wananchi, wafanyabiashara na wamiliki wa vibanda eneo la sokoni kwa nia ya kusikiliza kero zao na kuzitafutia ufumbuzi.

Katika mkutano huo uliochukua takribani masaa matatu Mkurugenzi aliwataka wananchi kutoa kero zao zote ili aone namna ya kuzitatua.

Katika mkutano huo kero kadhaa zilijitokeza zikiwemo ubovu wa choo, ukosefu wa sehemu ya kumwaga taka, mpangilio mzuri wa soko na tatizo la mikataba kati ya wamiliki wa vibanda na Manispaa ya Kinondoni.

Baada ya kuwasikiliza wananchi Mkurugenzi aliahidi kuwajengea choo cha kisasa, pia aliwaambia wananchi kuwa ukosefu wa sehemu ya kumwaga uchafu unakaribia kuisha. ''Manispaa ina mpango wa kujenga soko la kisasa jambo ambalo litaondoa kero mbili kwa wakati mmoja. Soko la kisasa likijengwa kwanza litakuwa na mpangilio mzuri na litakuwa na sehemu maalum ya kutupa na kumwaga taka" Alisema Kayombo

Aidha Mkurugenzi aliwaasa wananchi kuwa makini pindi wanavyotaka kufanya ujenzi ili kuepuka ujenzi holela. Aliwaambia ofisi ya Mkurugenzi kupitia idara ya Mipango miji, Ardhi na Ujenzi ipo wazi kwa mtu yoyote atakaehitaji msaada au ushauri kuhusiana na masuala mazima ya ujenzi.

Tangu kuanza kwa Manispaa ya Ubungo Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo amekuwa akitembelea wananchi wake kusikiliza kero na hatimaye kuzitafutia ufumbuzi ili kuleta maendeleo katika Manispaa yake.

Mimi ni wa tofauti, siwezi kukaa kwenye ma AC yale ofisini wakati wananchi wangu wanapata shida na wana kero nyingi. Lazima nitembee ili nijionee mwenyewe na hatimaye kuzitatua ndio maana hata hizi mvua haziwezi kuzuia mimi na wataalam wangu kuendelea na ziara. Tutazunguka pamoja na kulowa pamoja. Aliongeza Kayombo
Mkurugenzi aliwaambia wananchi kwamba soko lote la Sinza na vibanda vyake ni mali ya Manispaa ya Ubungo chini ya uangalizi wa Mkurugenzi hivyo wapangaji wote wanapaswa kuingia mkataba na Manispaa na sio mtu mwingine. Aliongeza kuwa vibanda vyote 204 vinavyozunguka soko sasa vitakuwa mali ya Manispaa na si vinginevyo ila wale watakaovihitaji basi wafuate utaratibu ili kuingia mikataba mizuri na Manispaa. 

Watakaofanikiwa kupata vibanda kwa kuingia mkataba na Manispaa watajipatia fursa ya kufanya biashara na kujiingizia kipato. Si hivyo tuu na Manispaa nayo itajiongezea kipato kupitia kodi ya pango na ushuru wa kila siku.

Alisema kwamba Manispaa imeamua kurudisha mali zake ili serikali iweze kukusanya mapato ya kutosha kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya maendeleo.

Aliwaomba wamiliki wa vibanda na wapangaji kufika ofisi ya Mkurugenzi iliyopo Kibamba ili waweze kufikia muafaka wa mikataba ya upangishwaji na taratibu zitakazofuata baada ya vibanda kuwa chini ya Manispaa.

Katika hatua nyingine Mkurugenzi aliwataka wamiliki 20 wa gereji katika eneo la Umma kinyume na utaratibu kufika katika ofisi ya Mkurugenzi Jumatatu saa mbili ili waweze kushauriwa kuhusu eneo la kuhamia au vinginevyo.

Mwisho Mkurugenzi aliwashukuru wananchi kwa kujitokeza na kuwaomba kuishi na kufanya biashara kwa amani kwa mustakabali wa maendeleo ya taifa letu.

Maoni