RC MAKONDA: TUSIPIMANE UBAVU.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Paul Makonda amewatahadharisha wanaume wanaodhani wanaweza kukaidi wito wa kufika ofisini kwake baada ya kulalamikiwa kutelekeza watoto ambapo amewatumia salamu kwa kuwaambia wasimjaribu wala kupima mamlaka aliyonayo. 

RC Makonda ametoa kauli hiyo wakati wa mahojiano ya kipindi cha tathimini ya Zoezi la kudai haki za watoto waliotelekezwa ambapo amesema tangu jumatatu zaidi ya 17,000 walifika ofisini kwake na Kati ya hao 4,400 wamesikilizwa. 

Aidha RC Makonda amesema kinachomfariji ni kuona idadi kubwa ya kinababa wanaofika ofisini kwake wanakubali kumlea mtoto ambapo hadi sasa familia 295 zimekubali kuhudumia mtoto na familia 29 zimepima DNA. 

Hata hivyo RC Makonda amesema baada ya zoezi hilo ataunda tume ya kuangalia changamoto zilizopo katika sheria ya matunzo ya mtoto kisha kuifikisha kwa waziri husika kwaajili ya kufikishwa Bungeni kwaajili kufanyiwa marekebisho.

Pamoja na hayo RC Makonda amesema hatoyumbishwa na baadhi ya watu wasiojua uchungu wanaopata kinamama kwa kubeza zoezi hilo kwakuwa yeye ametambua Mateso waliyokuwa wakipata kinamama waliotelekezwa. 

RC Makonda amesema ikitokea mwanamke aliefika ofisini kwake na kumshitaki mwanaume aliezaanae kisha uchunguzi ukafanyika na kubaini udanganyifu mwanaume anayo haki ya kufungua kesi ya kudhalilishwa na afisa ustawi wa jamii wa mkoa atalazimika kuwa shahidi mahakamani.

WATU WENYE DHAMBI WANAPENDA GIZA NDIO MAANA UKIWASHA NURU WANAIBUKA KUPINGA.

Maoni