RPC MJINI MAGHARIBI - NAWATAKA KTV WAFIKE KITUO CHA POLISI KWA HATUA ZA KISHERIA

Kufuatia kusambaa kwa taarifa iliyotolewa na kituo cha habari cha K TV kilichopo Kiembe samaki Unguja inayomtuhumu kijana aliyejitambulisha kwa jina la Ustadh Issa, kufanya vitendo vya udhalilishaji kwa watoto, Jeshi la Polisi mkoa wa Mjini Magharib Unguja limesema litawakamata watendaji wote wa K TV kufuatia taarifa zao ambazo mara nyingi hazina ushahidi.

Akizungumza na waandishi wa habari Kamanda wa Polisi mkoani hapo Hassan Nassir amewataka waandishi wa KTV waliohusika kutoa taarifa hiyo wafike kituo cha Polisi Madema kwa hatua za kisheria kwa kosa la kumtuhumu na kumdhalilisha kijana huyo.

Kamanda Nassir amesema wameanza kutia shaka utendaji kazi wa chombo hicho kutokana na tukio hilo si la kwanza “ wiki chache zilizopita KTV walitoa taarifa kama hiyo kwa kumpiga picha mwanamume mmoja akiwa chumbani na Mwanamume mwenziwe wamekaa kitandani wanaongea na kusambaza picha hiyo wakiwanadi kuwa ni mabarazuli” .

kwaupande wake Ustadh Issa ameiambia ZBC radio kuwa “ nilikuwa nimekaa maeneo ya Kidongo Chekundu akatokea mama mmoja, mwanamke na mtoto ambao walinitolea maneno mabaya na kunituhumu kutaka kumpa Tsh/20,000 mtoto wao ili kumfanyia vitendo vya udhalilishaji, walinichukuwa na kuwapigia cm K TV ambao walinihoji na nikapelekwa kituo cha polisi Ng’ambu baada ya mahojiano mtoto alithibitisha kuwa hajafanyiwa kitu chochote”.

Ustadh Issa ambaye amebainisha kuwa na mke na mtoto amesema kitendo cha K TV kutoa habari hiyo pasi na kuwa na ushahidi na kusambaa kwenye mitandao ya kijamii ni kumdhalilisha na kimemuondolea heshma yake kwa jamiii.

Maoni