UJENZI WA UKUTA MERERANI WAOKOA MAMILIONI - MAJALIWA


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema kukamilika kwa ujenzi wa ukuta kuzunguka mgodi wa Mirerani kutasaidia kuongeza mapato ya Serikali ikiwa ni pamoja na kudhibiti vitendo vya wizi na utoroshaji wa madini yaTanzanite. 

Ametoa kauli hiyo Jumanne, Aprili 10, 2018 Bungeni mjini Dodoma kwenye mkutano wa 11 wa Bunge, wakati akihitimisha mjadala wa mapitio ya utekelezaji wa kazi za Serikali kwa mwaka 2017/2018 na mwelekeo wa kazi za Serikali kwa mwaka 2018/2019. 

Waziri Mkuu amesema kukamilika kwa ujenzi wa ukuta huo uliozinduliwa Aprili 6, mwaka huu Rais Dkt. John Pombe Magufuli, kutasaidia pia kudhibiti ulanguzi na biashara ya magendo pamoja na kuimarisha usalama kwenye mgodi, kwa wafanyakazi na wafanyabiashara wa Tanzanite. 

“Kukamilika kwa ujenzi huo pia kutasaidia kuongeza mapato ambapo katika kipindi cha Januari hadi Machi 2018, Serikali imekusanya takriban shilingi milioni 714 ikilinganishwa na makusanyo ya shilingi milioni 147.1 kwa mwaka mzima wa 2017,” alisema. 

Waziri Mkuu alisema kabla ya ujenzi huo, inakadiriwa kuwa asilimia 40 ya madini ya Tanzanite yaliyokuwa yanazalishwa kila mwaka, yalitoroshwa kwa njia za panya na Serikali yetu haikuambulia chochote. “Hii ni kutokana na kukosekana udhibiti wa kutosha wa madini ya tanzanite kuanzia kwenye uzalishaji hadi kwa wauzaji,” alisema. 

Alisema mbali na kuwepo kwa eneo la wachimbaji ndani ya ukuta wa Mererani, pia kutajengwa maduka yaTanzanite na viwanda vya kuongeza thamani, hususan vya ukataji, uchongaji na ung’arishaji. Vilevile, kutakuwa na maeneo ya burudani ambayo yatastawisha zaidi biashara ya Tanzanite na kuwavuta watalii wengi kwenda kutembelea eneo hilo.

Maoni