WANANCH WA KIJIJI CHA MATAMBA WILAYANI MAKETE WAMEIBUKA SUALA LA UBOVU WA BARABARA.

Wananchi wa kijiji cha Matamba wilayani Makete mkoani Njombe wameibua suala la ubovu wa barabara ya Chimala Matamba na kuomba moyo waliokuwa nao awali wa kuchangia shughuli za maendeleo urudi tena. 

Katika mkutano wa hadhara uliofanyika hivi karibuni kijijini hapo, mwananchi mmoja amesema wamekuwa wakipata tabu wakati wa masika hivyo kuwaomba wananchi wenzake kuwa na moyo wa kujitoa kama awali Wakiongozwa na viongozi wao ili wafanye maendeleo kwenye yale maeneo korofi. 

Amesema mwanzoni kila mwananchi alikuwa akijitolea kwa kadri ya uwezo wake kuhakikisha wanakarabati maeneo korofi kwa kuwa wao ndio wanaopata tabu, lakini kwa sasa kila mtu anakuwa kimya. 

Diwani wa kata ya Matamba Mh Epheli Ng'ondya amesema tayari halmashauri imempatia kazi hiyo mkandarasi wa kutengeneza barabara hiyo na ataanza kazi rasmi pindi mvua zitakapomalizika

Pia amesema kwa kuwa mwananchi huyo ametoa wazo la kukarabati maeneo korofi kama walivyokuwa wanafanya siku zilizopita, yeye amelichukua wazo hilo na atatafuta wadau kwa kushirikiana na wananchi hao ili watekeleze suala. 

Naye diwani wa viti maalum Kata ya Mlondwe Mh Jeni Mbogela amewataka wananchi hao kushikamana kwa pamoja kwa kuwa ndiyo njia pekee ya kuleta maendeleo katika masuala mbalimbali ikiwemo barabara na sio kuisubiri serikali peke yake ifanye. 

Amesema endapo wakiamua kufanya shughuli za maendeleo serikali ikikuta wameanza ndiyo itatoa msaada na hapo ndipo maendeleo yanapoleta tija kwa wananchi. 

Chanzo : Green fm. 

Maoni